Yeremia 16:1-9
1
Kisha neno la Bwana likanijia:
2
“Kamwe usioe na kuwa na wana wala binti mahali hapa.”
3
Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana kuhusu wana na binti wazaliwao katika nchi hii, na kuhusu wale wanawake ambao ni mama zao, na wale wanaume ambao ni baba zao:
4
“Watakufa kwa magonjwa ya kufisha. Hawataombolezewa wala kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyosambaa juu ya ardhi. Watakufa kwa upanga na kwa njaa, nazo maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi.”
5
Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Usiingie katika nyumba ambayo kuna chakula cha matanga, usiende kuwaombolezea wala kuwahurumia, kwa sababu nimeziondoa baraka zangu, upendo wangu na huruma zangu kutoka kwa watu hawa,” asema Bwana.
6
“Wakubwa na wadogo watakufa katika nchi hii. Hawatazikwa wala kuombolezewa, na hakuna atakayejikatakata au kunyoa nywele za kichwa chake kwa ajili yao.
7
Hakuna yeyote atakayewapa chakula ili kuwafariji wale waombolezao kwa ajili ya wale waliokufa, hata akiwa amefiwa na baba au mama, wala hakuna yeyote atakayewapa kinywaji ili kuwafariji.
8
“Usiingie katika nyumba ambayo kuna karamu, na kuketi humo ili kula na kunywa.
9
Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli: ‘Mbele ya macho yako na katika siku zako, nitakomesha sauti zote za shangwe na za furaha, na pia sauti za bibi arusi na bwana arusi mahali hapa.’
Settings