Isaya 58:1-5
1
“Piga kelele, usizuie. Paza sauti yako kama tarumbeta. Watangazieni watu wangu uasi wao, na kwa nyumba ya Yakobo dhambi zao.
2
Kwa maana kila siku hunitafuta, wanaonekana kutaka kujua njia zangu, kana kwamba walikuwa taifa linalotenda lililo sawa, na ambalo halijaziacha amri za Mungu wake. Hutaka kwangu maamuzi ya haki, nao hutamani Mungu awakaribie.
3
Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona? Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’ “Lakini katika siku ya kufunga kwenu, mnafanya mnavyotaka na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote.
4
Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano, na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu. Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu.
5
Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua, siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza? Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete, na kwa kujilaza juu ya nguo ya gunia na majivu? Je, huo ndio mnaouita mfungo, siku iliyokubalika kwa Bwana?
Settings