Skip to content
Ezekieli 11:1-12

Ezekieli 11:1-12

1
Ndipo Roho akaniinua na kunileta mpaka kwenye lango la nyumba ya Bwana linalotazama upande wa mashariki. Pale kwenye ingilio la lango kulikuwepo wanaume ishirini na watano, nami nikaona miongoni mwao Yaazania mwana wa Azuri na Pelatia mwana wa Benaya, viongozi wa watu.
2
Bwana akaniambia, “Mwanadamu, hawa ndio wafanyao hila na kutoa mashauri potovu katika mji huu.
3
Wao husema, ‘Je, hivi karibuni hautakuwa wakati wa kujenga nyumba? Mji huu ni chungu cha kupikia, nasi ndio nyama.’
4
Kwa hiyo toa unabii dhidi yao, tabiri, Ewe mwanadamu.”
5
Kisha Roho wa Bwana akaja juu yangu, naye akaniambia niseme: “Hili ndilo Bwana asemalo: Hili ndilo ninyi mnalosema, ee nyumba ya Israeli, lakini ninajua mnalowaza mioyoni mwenu.
6
Mmewaua watu wengi katika mji huu na kujaza barabara zake maiti.
7
“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: maiti ulizozitupa huko ni nyama na mji huu ni chungu, lakini nitawaondoa mtoke huko.
8
Mnaogopa upanga, nao upanga huo ndio nitakaouleta juu yenu, asema Bwana Mwenyezi.
9
Nitawaondoa mtoke katika mji na kuwatia mikononi mwa wageni nami nitawaadhibu.
10
Mtaanguka kwa upanga, nami nitatimiza hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana.
11
Mji huu hautakuwa chungu kwa ajili yenu, wala hamtakuwa nyama ndani yake. Nitatoa hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli.
12
Nanyi mtajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana, kwa kuwa hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu, bali mmefuata mwenendo wa mataifa yanayowazunguka.”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options