Skip to content
Kumbukumbu 9:18-29

Kumbukumbu 9:18-29

18
Ndipo tena nikasujudu mbele za Bwana kwa siku arobaini usiku na mchana. Sikula mkate wala sikunywa maji, kwa sababu ya dhambi yote mliyoifanya, mkifanya lile lililo ovu mbele za Bwana na kumkasirisha.
19
Niliogopa hasira na ghadhabu ya Bwana, kwa kuwa aliwakasirikia vya kutosha na kutaka kuwaangamiza. Lakini Bwana alinisikiliza tena.
20
Bali yeye alimkasirikia Aroni kiasi cha kutaka kumwangamiza, nami wakati huo nilimwombea Aroni pia.
21
Kisha nikachukua ile sanamu ya ndama mliyoitengeneza na kuichoma kwenye moto. Nikaiponda na kuisaga ikawa unga laini kama vumbi, nikatupa lile vumbi kwenye kijito kilichotiririka toka mlimani.
22
Pia mlimkasirisha Bwana huko Tabera, Masa na Kibroth-Hataava.
23
Vilevile wakati Bwana alipowatuma kutoka Kadesh-Barnea, alisema, “Kweeni, mkaimiliki nchi ambayo nimewapa.” Lakini mliasi dhidi ya agizo la Bwana Mungu wenu. Hamkumtegemea wala kumtii.
24
Mmekuwa waasi dhidi ya Bwana tangu nilipowajua ninyi.
25
Nilianguka kifudifudi mbele za Bwana kwa zile siku arobaini usiku na mchana kwa sababu Bwana alikuwa amesema angewaangamiza ninyi.
26
Nilimwomba Bwana na kusema, “Ee Bwana Mwenyezi, usiangamize watu wako, urithi wako mwenyewe ule ulioukomboa kwa uweza wako mkuu na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu.
27
Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Yakobo. Usiangalie ukaidi wa watu hawa, uovu wao wala dhambi yao.
28
Watu wa nchi ile uliyotutoa sisi wasije wakasema, ‘Ni kwa sababu Bwana hakuweza kuwachukua mpaka nchi aliyokuwa amewaahidia, kwa sababu aliwachukia, akawaleta ili aje kuwaua jangwani.’
29
Bali wao ni watu wako, urithi wako ule ulioutoa Misri kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyooka.”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Reading Width 45 chars

Options