Skip to content
Kumbukumbu 28:33-57

Kumbukumbu 28:33-57

33
Taifa usilolijua watakula mazao ya nchi yako na taabu ya kazi yako, hutakuwa na chochote, bali kuonewa kikatili siku zako zote.
34
Vitu utakavyoviona kwa macho yako vitakufanya wazimu.
35
Bwana atayapiga magoti yako na miguu yako kwa majipu yenye maumivu makali yasiyoponyeka, yakienea kutoka nyayo za miguu yako hadi utosini.
36
Bwana atakupeleka wewe na mfalme uliyemweka juu yako uende kwenye taifa ambalo hukulijua wewe wala baba zako. Huko utaabudu miungu mingine, miungu ya miti na mawe.
37
Utakuwa kitu cha kuchukiza, tena kitu cha kudharauliwa na kudhihakiwa kwa mataifa yote huko Bwana atakakokupeleka.
38
Utapanda mbegu nyingi katika shamba lakini utavuna haba, kwa sababu nzige watazila.
39
Utapanda mashamba ya mizabibu na kuyapalilia, lakini hutakunywa divai yake wala hutakusanya zabibu, kwa sababu wadudu watazila.
40
Utakuwa na mizeituni katika nchi yako yote, lakini hutatumia hayo mafuta yake, kwa sababu zeituni zitapukutika.
41
Utakuwa na wana na binti lakini hawatakuwa nawe, kwa sababu watachukuliwa mateka.
42
Makundi ya nzige yatavamia miti yako yote na mazao ya nchi yako.
43
Mgeni anayeishi miongoni mwako atainuka juu zaidi na zaidi kuliko wewe, lakini wewe utashuka chini zaidi na zaidi.
44
Yeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha. Yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia.
45
Laana hizi zote zitakuja juu yako. Zitakufuatia na kukupata mpaka uangamizwe, kwa sababu hukumtii Bwana Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake aliyokupa.
46
Zitakuwa ishara na ajabu kwako na kwa wazao wako milele.
47
Kwa sababu hukumtumikia Bwana Mungu wako kwa furaha na kwa moyo wakati wa kufanikiwa kwako,
48
kwa hiyo katika njaa na kiu, katika uchi na umaskini wa kutisha, utawatumikia adui ambao Bwana atawatuma dhidi yako. Yeye ataweka nira ya chuma shingoni mwako hadi amekwisha kukuangamiza.
49
Bwana ataleta taifa dhidi yako kutoka mbali, kutoka miisho ya dunia, kama tai ashukiavyo mawindo chini, taifa ambalo hutaijua lugha yake,
50
taifa lenye uso mkali lisilojali wazee wala kuwahurumia vijana.
51
Watakula wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako mpaka umeangamia. Hawatakuachia nafaka, divai mpya au mafuta, wala ndama wowote wa kundi lako au wana-kondoo wa kundi lako mpaka umekuwa magofu.
52
Nao wataizingira miji yote katika nchi yako mpaka kuta ndefu za ngome ambazo unazitegemea zimeanguka. Watazingira miji yote katika nchi ambayo Bwana Mungu wako anakupa.
53
Utakula uzao wa tumbo lako, nyama ya wana wako na binti zako ambao Bwana Mungu wako amekupa, kwa sababu ya mateso yale adui zako watakayokuletea wakati wa kukuzingira.
54
Hata yule mtu muungwana sana na makini miongoni mwako hatakuwa na huruma kwa ndugu yake mwenyewe au kwa mke ampendaye au watoto wake waliosalia,
55
naye hatampa hata mmoja wao nyama ya watoto wake ambao anawala. Kwa kuwa hakuna kitu kingine kilichosalia kwake katika mazingirwa makali ambayo adui yako watakuletea kwa miji yako yote.
56
Mwanamke ambaye ni muungwana sana na makini miongoni mwako, yaani ambaye ni makini sana na muungwana kiasi kwamba asingethubutu kugusa ardhi kwa wayo wa mguu wake, yeye atakuwa mchoyo kwa mume ampendaye na mwanawe mwenyewe au binti yake,
57
kondoo wa nyuma kutoka kwenye tumbo lake na watoto anaowazaa. Kwa kuwa anakusudia kuwala kwa siri wakati wa kuzingirwa na katika taabu zile ambazo adui yako atazileta juu yako na miji yako.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options