Skip to content
Kumbukumbu 1:19-40

Kumbukumbu 1:19-40

19
Kisha, kama Bwana Mungu wetu alivyotuamuru, tuliondoka kutoka Horebu na kwenda kuelekea nchi ya vilima ya Waamori, kupitia jangwa lile kubwa lote la kutisha, lile mliloliona, nasi tukafika Kadesh-Barnea.
20
Kisha niliwaambia, “Mmefika katika nchi ya vilima ya Waamori, ambayo Bwana Mungu wetu anatupa.
21
Tazama, Bwana Mungu wenu amewapa nchi. Pandeni mkaimiliki kama Bwana, Mungu wa baba zenu, alivyowaambia. Msiogope, wala msikate tamaa.”
22
Ndipo ninyi nyote mkanijia na kusema, “Tupeleke watu watutangulie kuipeleleza nchi kwa ajili yetu, na kutuletea taarifa kuhusu njia tutakayopita, na miji tutakayoiendea.”
23
Wazo hilo lilionekana zuri kwangu; kwa hiyo niliwachagua watu wenu kumi na wawili, mwanaume mmoja kutoka kila kabila.
24
Waliondoka na kukwea katika nchi ya vilima, wakafika katika Bonde la Eshkoli na kuipeleleza.
25
Wakachukua baadhi ya matunda ya nchi, wakatuletea na kutuarifu, “Ni nchi nzuri ambayo Bwana Mungu wetu anatupa.”
26
Lakini hamkuwa tayari kukwea, mkaasi dhidi ya amri ya Bwana Mungu wenu.
27
Mkanungʼunika ndani ya mahema yenu na kusema, “Bwana anatuchukia, kwa hiyo alitutoa Misri ili kututia mikononi mwa Waamori kutuangamiza.
28
Twende wapi? Ndugu zetu wametufanya kufa moyo. Wanasema, ‘Watu wa huko wana nguvu zaidi na ni warefu kuliko sisi tulivyo; miji ni mikubwa, yenye kuta zilizofika juu angani. Zaidi ya hayo, tumewaona Waanaki huko.’ ”
29
Ndipo nikawaambia, “Msihofu, wala msiwaogope.
30
Bwana Mungu wenu anayewatangulia, atawapigania, kama alivyofanya kwa ajili yenu huko Misri, mbele ya macho yenu hasa,
31
na pia huko jangwani. Huko mliona jinsi Bwana Mungu wenu alivyowachukua, kama baba amchukuavyo mwanawe, katika njia yote mliyoiendea mpaka mkafika mahali hapa.”
32
Pamoja na hili, hamkumtegemea Bwana Mungu wenu,
33
ambaye aliwatangulia katika safari yenu, kwa moto usiku na kwa wingu mchana, kuwatafutia mahali penu pa kupiga kambi na kuwaonyesha njia mtakayoiendea.
34
Wakati Bwana aliposikia lile mlilosema, alikasirika, akaapa, akasema:
35
“Hakuna mtu wa kizazi hiki kiovu atakayeona nchi nzuri niliyoapa kuwapa baba zenu,
36
isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune. Yeye ataiona, nami nitampa yeye na wazao wake nchi aliyoikanyaga kwa miguu, kwa sababu alimfuata Bwana kwa moyo wote.”
37
Kwa sababu yenu Bwana pia alinikasirikia mimi, akasema, “Hutaingia hiyo nchi pia.
38
Lakini msaidizi wako, Yoshua mwana wa Nuni, ataingia. Mtie moyo, kwa sababu atawaongoza Waisraeli kuirithi hiyo nchi.
39
Wale watoto ambao mliwasema wangelichukuliwa mateka, yaani watoto wenu ambao bado hawajui jema na baya, wataingia katika nchi. Nitawapa hiyo nchi, nao wataimiliki.
40
Bali ninyi geukeni, mwondoke kuelekea jangwani kwa kufuata njia ya Bahari ya Shamu.”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options