Matendo 26:4-11
4
“Wayahudi wote wanajua jinsi nilivyoishi tangu nilipokuwa mtoto, kuanzia mwanzo wa maisha yangu katika nchi yangu na pia huko Yerusalemu.
5
Wao wamefahamu kwa muda mrefu na wanaweza kushuhudia kama wakipenda, ya kwamba kutokana na misimamo mikali sana ya dhehebu letu kwenye dini yetu, niliishi nikiwa Farisayo.
6
Nami sasa ni kwa sababu ya tumaini langu katika kile ambacho Mungu aliwaahidi baba zetu, ninashtakiwa leo.
7
Hii ndiyo ahadi ambayo makabila yetu kumi na mawili yanatarajia kuiona ikitimizwa wanapomtumikia Mungu kwa bidii usiku na mchana. Ee mfalme, ninashtakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hili.
8
Kwa nini yeyote miongoni mwenu afikiri kwamba ni jambo lisilosadikika Mungu kufufua wafu?
9
“Mimi pia nilikuwa nimeshawishika kwamba imenipasa kufanya yote yale yaliyowezekana kupinga Jina la Yesu wa Nazareti.
10
Nami hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Kwa mamlaka ya viongozi wa makuhani, niliwatia wengi wa watakatifu gerezani na walipokuwa wakiuawa, nilipiga kura yangu kuunga mkono.
11
Mara nyingi nilikwenda kutoka sinagogi moja hadi ingine nikiamuru waadhibiwe, nami nilijaribu kuwalazimisha wakufuru. Katika shauku yangu dhidi yao, hata nilikwenda miji ya kigeni ili kuwatesa.
Settings