Matendo 2:14-21
14
Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akainua sauti yake na kuhutubia ule umati wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, jueni jambo hili mkanisikilize.
15
Hakika watu hawa hawakulewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi!
16
La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:
17
“ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu na binti zenu watatabiri, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.
18
Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu, nao watatabiri.
19
Nami nitaonyesha maajabu juu mbinguni, na ishara chini duniani: damu, moto, na mawimbi ya moshi.
20
Jua litakuwa giza na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana iliyo tukufu.
21
Na kila mtu atakayeliitia jina la Bwana, ataokolewa.’
Settings