2 Nyakati 7:12-22
12
Bwana akamtokea Solomoni usiku na kumwambia: “Nimesikia maombi yako nami nimechagua mahali hapa kwa ajili yangu mwenyewe kuwa Hekalu kwa ajili ya dhabihu.
13
“Wakati nitakapofunga mbingu ili isiwepo mvua, au nikiamuru nzige kula mazao ya nchi au nikituma tauni miongoni mwa watu wangu,
14
kama watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao na nitaiponya nchi yao.
15
Sasa macho yangu yatafumbuka na masikio yangu yatasikiliza kwa makini maombi yaombwayo mahali hapa.
16
Kwa maana sasa nimechagua na kutakasa Hekalu hili ili kwamba Jina langu lipate kuwa huko milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwepo huko daima.
17
“Kwa habari yako wewe, kama ukienenda mbele zangu kama Daudi baba yako alivyoenenda na kufanya yote nikuamuruyo, nawe ukizishika amri zangu na sheria zangu,
18
Nitakiimarisha kiti chako cha enzi kama nilivyoagana na Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe mtu wa kutawala juu ya Israeli.’
19
“Lakini kama ukigeuka na kuyaacha maagizo na amri nilizowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,
20
ndipo nitakapoingʼoa Israeli kutoka nchi yangu niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Nitalifanya kitu cha kudharauliwa na kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote.
21
Ingawa Hekalu hili linavutia sana sasa, wote watakaolipita watashangaa na kusema, ‘Kwa nini Bwana amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’
22
Watu watajibu, ‘Ni kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewatoa Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu ameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”
Settings