1 Samweli 14:36-45
36
Sauli akasema, “Tuteremke tufuatie Wafilisti usiku na kuwateka nyara mpaka mapambazuko, nasi tusiache hata mmoja wao hai.” Wakajibu, “Fanya lolote lile uonalo jema zaidi kwako.” Lakini kuhani akasema, “Tuulize kwa Mungu mahali hapa.”
37
Basi Sauli akamuuliza Mungu, akisema, “Je, niteremke kuwafuatia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Israeli?” Lakini Mungu hakumjibu siku ile.
38
Kwa hiyo Sauli akasema, “Njooni hapa, ninyi nyote ambao ni viongozi wa jeshi, na tutafute ni dhambi gani imefanywa leo.
39
Kwa hakika kama Bwana aiokoaye Israeli aishivyo, hata kama itakuwa juu ya mwana wangu Yonathani, ni lazima afe.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyesema neno.
40
Kisha Sauli akawaambia Waisraeli wote, “Ninyi simameni huko; mimi na mwanangu Yonathani tutasimama hapa.” Watu wakajibu, “Fanya lile unaloona jema zaidi kwako.”
41
Kisha Sauli akamwomba Bwana, Mungu wa Israeli, akisema, “Nipe jibu lililo sawa.” Yonathani na Sauli wakatolewa kwa kura, nao watu wakawa salama.
42
Sauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Kura ikamwangukia Yonathani.
43
Basi Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie ni nini ulichokifanya.” Hivyo Yonathani akamwambia, “Nilionja tu asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu. Je, sasa ni lazima nife?”
44
Sauli akasema, “Mungu na anishughulikie kwa ukali zaidi kama wewe Yonathani hutakufa.”
45
Lakini watu wakamwambia Sauli, “Je, Yonathani atakufa, yeye ambaye ameleta wokovu huu mkubwa Israeli? Hasha! Hakika kama Bwana aishivyo, hakuna hata unywele wa kichwa chake utakaoanguka juu ya ardhi, kwa kuwa alifanya jambo hili leo kwa msaada wa Mungu.” Basi watu wakamwokoa Yonathani, wala hakuuawa.
Settings