1 Nyakati 29:9-20
9
Watu wakafurahi kwa sababu ya itikio la hiari la viongozi wao, kwa kuwa walikuwa wametoa kwa hiari na kwa moyo wote kwa Bwana. Mfalme Daudi pia akafurahi sana.
10
Daudi akamhimidi Bwana mbele ya kusanyiko lote, akisema: “Uhimidiwe wewe, Ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu, tangu milele hata milele.
11
Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee Bwana, ufalme ni wako; umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.
12
Utajiri na heshima vyatoka kwako; wewe ndiwe utawalaye vitu vyote. Mikononi mwako kuna nguvu na uweza ili kuinua na kuwapa wote nguvu,
13
Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu Jina lako tukufu.
14
“Lakini mimi ni nani, nao watu wangu ni nani, hata tuweze kukutolea kwa ukarimu namna hii? Vitu vyote vyatoka kwako, nasi tumekutolea tu vile vitokavyo mkononi mwako.
15
Sisi ni wageni na wapitaji machoni pako, kama walivyokuwa baba zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli, bila tumaini.
16
Ee Bwana Mungu wetu, kwa wingi wote huu ambao tumekutolea kwa kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina lako Takatifu, vimetoka mkononi mwako, navyo vyote ni mali yako.
17
Ninajua, Mungu wangu, kwamba wewe huujaribu moyo na unapendezwa na unyofu. Vitu hivi vyote nimetoa kwa hiari na kwa moyo mnyofu. Nami sasa nimeona kwa furaha jinsi watu wako walioko hapa kwa hiari yao walivyokutolea wewe.
18
Ee Bwana, Mungu wa baba zetu Abrahamu, Isaki na Israeli, weka shauku hii ndani ya mioyo ya watu wako daima na uifanye mioyo yao iwe na uaminifu kwako.
19
Nawe umpe mwanangu Solomoni kujitolea kwako kwa moyo wote ili kuzishika amri zako, masharti yako, maagizo yako na kufanya kila kitu ili kujenga Hekalu hili la fahari ambalo kwa ajili yake nimetoa.”
20
Ndipo Daudi akaliambia kusanyiko lote, “Mhimidini Bwana Mungu wenu.” Hivyo wote wakamhimidi Bwana, Mungu wa baba zao. Wakasujudu na kuanguka kifudifudi mbele za Bwana na mfalme.
Settings