1 Nyakati 28:1-10
1
Daudi akawaita maafisa wote wa Israeli wakusanyike huko Yerusalemu: yaani, maafisa walio juu ya makabila, majemadari wa vikosi katika utumishi wa mfalme, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, maafisa wanaosimamia mali zote na mifugo ya mfalme na wanawe, wakiwemo maafisa wa jumba la kifalme, mashujaa na askari wote walio hodari.
2
Mfalme Daudi akainuka na kusema: “Nisikilizeni ndugu zangu nanyi watu wangu. Nilikuwa na nia ya kujenga nyumba ili iwe mahali pa kukaa Sanduku la Agano la Bwana kwa ajili ya kuwa mahali pa kuwekea miguu ya Mungu wetu, nami nikafanya maandalizi ya kuijenga.
3
Lakini Mungu akaniambia, ‘Wewe hutajenga nyumba kwa Jina langu, kwa sababu wewe umepigana vita na umemwaga damu.’
4
“Hata hivyo, Bwana, Mungu wa Israeli, alinichagua mimi kutoka jamaa yangu yote niwe mfalme juu ya Israeli milele. Alimchagua Yuda kuwa kiongozi na kutoka nyumba ya Yuda akaichagua jamaa yangu na kutoka wana wa baba yangu ikampendeza kunifanya niwe mfalme juu ya Israeli yote.
5
Miongoni mwa wanangu wote, naye Bwana amenipa wengi, amemchagua Solomoni mwanangu ili kukikalia kiti cha enzi cha ufalme wa Bwana juu ya Israeli.
6
Aliniambia, ‘Solomoni mwanao ndiye atakayejenga nyumba yangu na nyua zangu, kwa maana nimemchagua yeye kuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake.
7
Nitaufanya imara ufalme wake milele kama akiendelea kuzishika amri zangu na sheria zangu, kama afanyavyo hivi leo.’
8
“Hivyo basi ninawaagiza mbele za Israeli yote na kusanyiko hili la Bwana naye Mungu wetu akiwa anasikia: Kuweni na bidii kuzifuata amri za Bwana Mungu wenu, ili mpate kumiliki nchi hii nzuri na kuwaachia wana wenu kuwa urithi milele.
9
“Nawe Solomoni mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa kujitoa kwa moyo wote na kwa nia ya kumkubali, kwa maana Bwana huuchunguza kila moyo na kujua kila kusudi la kila fikira. Ukimtafuta, ataonekana kwako; bali kama ukimwacha, yeye atakukataa milele.
10
Angalia basi, kwa maana Bwana amekuchagua wewe ili ujenge Hekalu kuwa mahali patakatifu. Uwe hodari ukafanye kazi hiyo.”
Settings