Walawi 24:10-23
10
Basi mwana wa mama Mwisraeli na baba Mmisri alikwenda miongoni mwa Waisraeli, nayo mapigano yakatokea ndani ya kambi kati yake na Mwisraeli.
11
Huyu mwana wa mwanamke Mwisraeli akalikufuru Jina la Bwana kwa kulaani; kwa hiyo wakamleta kwa Mose. (Jina la mama yake aliitwa Shelomithi binti wa Dibri, wa kabila la Dani.)
12
Nao wakamweka mahabusu mpaka mapenzi ya Bwana yawe wazi kwao.
13
Ndipo Bwana akamwambia Mose:
14
“Mchukue huyo aliyekufuru nje ya kambi. Wale wote waliomsikia akikufuru wataweka mikono juu ya kichwa chake, kisha kusanyiko lote litampiga mawe.
15
Waambie Waisraeli: ‘Ikiwa mtu yeyote atamlaani Mungu wake, atakuwa na hatia kwa uovu wake;
16
yeyote atakayekufuru Jina la Bwana ni lazima auawe. Kusanyiko lote litampiga kwa mawe. Iwe ni mgeni au mzawa, atakapolikufuru Jina la Bwana, ni lazima auawe.
17
“ ‘Kama mtu yeyote atamuua mtu mwingine, ni lazima auawe.
18
Mtu yeyote auaye mnyama wa mtu mwingine lazima afidie, uhai kwa uhai.
19
Ikiwa mtu yeyote atamjeruhi jirani yake, chochote alichomtenda naye atatendewa:
20
iwapo amemvunja mfupa atavunjwa mfupa, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kama alivyomjeruhi mwenzake, vivyo hivyo ndivyo atakavyojeruhiwa.
21
Yeyote auaye mnyama wa mtu lazima alipe fidia, lakini yeyote auaye mtu, lazima auawe.
22
Mtakuwa na sheria iyo hiyo kwa mgeni na kwa mzawa. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”
23
Kisha Mose akasema na Waisraeli, nao wakamchukua yule aliyekufuru nje ya kambi na kumpiga mawe. Waisraeli wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Mose.
Settings