Skip to content
2 Nyakati 33:11-20

2 Nyakati 33:11-20

11
Hivyo Bwana akaleta juu yao majemadari wa jeshi la mfalme wa Ashuru, ambao walimchukua Manase kwenda kifungoni, wakaweka ndoana katika pua yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.
12
Katika dhiki yake akamsihi Bwana Mungu wake na kujinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake.
13
Naye alipomwomba, Bwana akaguswa na kule kusihi kwake na akasikiliza kilio chake, kwa hiyo akamrudisha Yerusalemu na kwenye ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kwamba Bwana ndiye Mungu.
14
Baadaye akajenga ukuta wa nje wa Mji wa Daudi, magharibi mwa chemchemi ya Gihoni katika bonde, hadi kufikia ingilio la Lango la Samaki na akakizunguka kilima cha Ofeli, pia akaufanya kuwa mrefu zaidi. Akawaweka majemadari katika miji yote ya Yuda iliyokuwa imejengewa ngome.
15
Akaondolea mbali miungu ya kigeni na kuondoa sanamu kutoka Hekalu la Bwana pamoja na madhabahu zote alizozijenga katika kile kilima kilichojengwa Hekalu na katika Yerusalemu, akazitupa nje ya mji.
16
Kisha akarudisha madhabahu ya Bwana na kutolea juu yake dhabihu za sadaka za amani pamoja na sadaka za shukrani, naye akawaamuru Yuda wamtumikie Bwana, Mungu wa Israeli.
17
Lakini hata hivyo watu wakaendelea kutoa dhabihu mahali pa juu pa kuabudia miungu, lakini wakimtolea Bwana Mungu wao peke yake.
18
Matukio mengine ya utawala wa Manase, maombi yake kwa Mungu wake na maneno aliyoambiwa na waonaji walionena naye kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
19
Maombi yake, pamoja na jinsi Mungu alivyoguswa na kusihi kwake, pia dhambi zake zote na kukosa kwake uaminifu pamoja na sehemu alizojenga mahali pa juu pa kuabudia miungu, kule kusimamisha nguzo za Ashera na sanamu kabla ya kujinyenyekeza kwake, yote yameandikwa katika kumbukumbu za waonaji.
20
Manase akalala pamoja na baba zake akazikwa katika jumba lake la kifalme. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options