1 Samweli 12:6-18
6
Kisha Samweli akawaambia watu, “Bwana ndiye alimchagua Mose na Aroni, na kuwaleta baba zenu akiwapandisha kutoka Misri.
7
Sasa basi, simameni hapa, kwa sababu nitakabiliana nanyi kwa ushahidi mbele za Bwana wa matendo yote ya haki yaliyofanywa na Bwana kwenu na kwa baba zenu.
8
“Baada ya Yakobo kuingia Misri, walimlilia Bwana kwa ajili ya msaada, naye Bwana akawatuma Mose na Aroni, ambao waliwatoa baba zenu kutoka Misri na kuwakalisha mahali hapa.
9
“Lakini wakamsahau Bwana Mungu wao, hivyo Mungu akawauza katika mkono wa Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori na katika mikono ya Wafilisti na mfalme wa Moabu, ambaye alipigana dhidi yao.
10
Wakamlilia Bwana na kusema, ‘Tumetenda dhambi; tumemwacha Bwana na kutumikia Mabaali na Maashtorethi. Lakini sasa tuokoe kutoka mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia.’
11
Ndipo Bwana akawatuma Yerub-Baali, Baraka, Yefta na Samweli, naye akawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu kila upande, ili ninyi mpate kukaa salama.
12
“Lakini mlipomwona yule Nahashi mfalme wa Waamoni anakuja dhidi yenu, mliniambia, ‘Hapana, tunataka mfalme atutawale,’ hata ingawa Bwana Mungu wenu alikuwa mfalme wenu.
13
Sasa huyu hapa ndiye mfalme mliyemchagua, yule mliyeomba; tazameni, Bwana amemweka mfalme juu yenu.
14
Kama mkimcha Bwana na kumtumikia na kumtii nanyi msipoasi dhidi ya amri zake, ninyi pamoja na mfalme anayetawala juu yenu mkimfuata Bwana, Mungu wenu, mambo yatakuwa mema kwenu!
15
Lakini kama hamkumtii Bwana, nanyi kama mkiasi dhidi ya amri zake, mkono wake utakuwa dhidi yenu, kama ulivyokuwa dhidi ya baba zenu.
16
“Sasa basi, simameni kimya mkaone jambo hili kubwa ambalo Bwana anakwenda kulifanya mbele ya macho yenu!
17
Je, sasa si mavuno ya ngano? Nitamwomba Bwana ili alete ngurumo na mvua. Nanyi mtatambua jambo hili lilivyo baya mlilolifanya mbele za macho ya Bwana mlipoomba mfalme.”
18
Kisha Samweli akamwomba Bwana, na siku ile ile Bwana akatuma ngurumo na mvua. Hivyo watu wote wakamwogopa sana Bwana na Samweli.
Settings