1 Nyakati 29:1-9
1
Ndipo Mfalme Daudi akaliambia kusanyiko lote: “Mwanangu Solomoni, yeye ambaye Mungu amemchagua, ni kijana mdogo na asiye na uzoefu. Kazi hii ni kubwa, kwa sababu Hekalu hili la fahari si kwa ajili ya mwanadamu bali ni kwa ajili ya Bwana.
2
Kwa uwezo wangu wote nimetenga mali kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu: dhahabu kwa kazi za dhahabu, fedha kwa ajili ya fedha, shaba kwa kazi za shaba, chuma kwa kazi za chuma na miti kwa kazi za miti, vivyo hivyo vito vya shohamu kwa ajili ya kutia kwenye vijalizo, almasi, mawe ya rangi mbalimbali, aina zote za vito vya thamani na marmar; yote haya kwa wingi mno.
3
Zaidi ya hayo, kwa kujitolea kwangu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, sasa ninatoa hazina zangu mwenyewe za dhahabu na fedha kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, zaidi ya mali niliyotoa kwa ajili ya Hekalu hili takatifu:
4
talanta 3,000 za dhahabu (dhahabu ya Ofiri) na talanta 7,000 za fedha safi iliyosafishwa, kwa ajili ya kufunika kuta za Hekalu,
5
kwa kazi ya dhahabu na kazi ya fedha na kwa kazi yote itakayofanywa na mafundi. Basi, ni nani anayependa kujitoa kwa Bwana leo?”
6
Ndipo viongozi wa jamaa, maafisa wa kabila za Israeli, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, pamoja na maafisa waliokuwa wasimamizi wa kazi za mfalme wakatoa kwa hiari yao.
7
Wakatoa kwa ajili ya kazi ya Hekalu la Mungu talanta 5,000 na darkoni 10,000 za dhahabu, talanta 10,000 za fedha, talanta 18,000 za shaba na talanta 100,000 za chuma.
8
Kila mmoja aliyekuwa na vito vya thamani akavitoa katika hazina ya Hekalu la Bwana chini ya uangalizi wa Yehieli Mgershoni.
9
Watu wakafurahi kwa sababu ya itikio la hiari la viongozi wao, kwa kuwa walikuwa wametoa kwa hiari na kwa moyo wote kwa Bwana. Mfalme Daudi pia akafurahi sana.
Settings